Usawa Kwenye Sheria? Sio kwa CBC au FinCEN

Julai 20, 2016

Mwishoni mwa wiki iliyopita ilitangazwa na Benki Kuu ya Cyprus (CBC) kwamba Benki ya Hellenic, taasisi ya fedha iliyosajiliwa katika Jamhuri ya Cyprus, walikiuka sheria ya kupambana na fedha chafu na kufadhili magaidi, na wajibu wa ‘kumjua-mteja wako’. Mapungufu haya au udhaifu, CBC imesema, yameonekana “… kwenye ukaguzi wa ndani uliofanywa Septemba 2014, kuchunguza shughuli za Benki ya Hellenic katika miaka iliyotangulia.”

Adhabu: Faini ya Euro 1,100,000 na ahadi kutoka Hellenic kuonyesha kwamba wataboresha mifumo yao. Taarifa hiyo iliongeza kwamba Benki ya Hellenic, taasisi inayomilikiwa na Wacyprus, pia itaweza kufaidika na punguzo la 15% ya adhabu iwapo itatoa ushirikiano kwa CBC. Pia Hellenic imefunga akaunti 8,000 kwa kuzingatia taratibu za CBC.

Ukilinganisha hili na vitendo vya CBC karibu miaka miwili iliyopita wakati walipoituhumu FBME kwa udhaifu kama huo. Badala ya faini, CBC ilitumia sheria mbovu ya kulichukua tawi la Cyprus la Benki ya FBME, inayomilikiwa na Walebanoni na kusajiliwa Tanzania. Walisimamisha shughuli zote za Benki kwa muda wa wiki sita, kuharibu uendeshaji wa idara tanzu ambayo haikuwa na tuhuma zozote, kusababisha madhara makubwa kwa wateja na kuzuia upatikanaji wa fedha zao na kujaribu kulitaifisha tawi tangu mwishoni mwa mwaka 2015. Juu ya hayo, walitoza faini ya € 1,200,000 kwa FBME, na hakuna punguzo lolote lililotolewa wala ofa ya ushirikiano na Benki. Kwa hali yoyote, FBME imegomea faini hiyo kwa kulipelekwa jambo hili mahakama ya sheria nchini Cyprus ambako bado inaendelea. Hakuna akaunti iliyofungwa kwa FBME na kuwekwa chini ya udhibiti wa CBC.

Na kubwa zaidi kwenye hili ni kwamba hatua dhidi ya FBME na wateja wake ilitegemea ripoti ambayo haikuwa sahihi na baadae kuonekana ya kupikwa!

Wakati huo huo, CBC imeshindwa kuonyesha ushahidi wa maandishi kuthibitisha hatua yake ya kibabe dhidi ya FBME. Ni muhimu pia kutambua kwamba dhana ya hatia iliyotolewa na CBC dhidi ya FBME haikubaliani na chunguzi mbalimbali zilizofanywa na wahasibu wa kimataifa.

Pia walio kimya kwenye kesi ya Benki ya Hellenic ni Financial Crimes Enforcement Network (FinCEN), wakala wa Idara ya hazina ya Marekani. Wachunguzi wa kesi ya FBME watakumbuka kwamba ilikuwa ni FinCEN waliosambaza madai Julai 2014 dhidi ya FBME, huku wakikataa kufichua ushahidi kuthibitisha tuhuma zake. Pingamizi la kisheria la FBME dhidi ya FinCEN bado linaendelea nchini Marekani.

Jinsi mambo yalivyo, hakuna maelezo ya kutosha ya kwa nini FinCEN imeshindwa kushughulikia kesi ya Benki ya Hellenic na mapungufu yake yaliyobainika ya kupambana na fedha chafu, wakati FinCEN inalazimisha adhabu kubwa kabisa dhidi ya Benki ya FBME bila kuwepo ushahidi ulio dhahiri.

Msingi mkuu wa kidemokrasia ni kwamba wote mnatendewa sawa chini ya sheria; kila mmoja anapaswa kutendewa haki kwa mujibu wa sheria hiyo. Hata hivyo msingi huo unakiukwa nchini Cyprus kwa waziwazi kabisa. Ni vihumu kupima ni vipi na kwa nini shutuma mbili zinazofanana, ya – kwanza dhidi ya FBME mwaka 2014 na ya pili mwaka 2016 dhidi ya Benki ya Hellenic kwa makosa yaliyofanyika miaka miwili na zaidi nyuma – kuwa na matokeo mawili yanayotofautiana kiasi hiki.

Na bado ni vigumu mno kuelewa kwa nini FBME inalazimika kupata adhabu ya kifo wakati Hellenic inapata faini nyepesi, ingawaje shutuma dhidi ya wa mwanzo ni za kutatanisha zaidi, wakati zile dhidi ya wa sasa hazipingiki.